Wakati Tanzania inatimiza miaka 60 ya uhuru wake ifikapo Desemba 9 mwaka huu, vyama vya upinzani ni miongoni mwa taasisi zinazoendelea kutoa mchango mkubwa katika siasa, pamoja na mijadala anuai inayogusa maeneo ya uchumi,haki za binadamu,asasi za kiraia,uhuru wa kujieleza kwa wananchi,wanasiasa na vyama vyenyewe pamoja na amani na maendeleo tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1992 nchini humo.
Duru za kisiasa zinasema kwa kutumia Bunge la nchi hiyo, Ibara ya 100(1) ya madaraka na Haki za Bunge, inayoagiza uhuru wa mawazo,majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru wake pamoja na majukwaa mengine ya kisiasa, vyama vya upinzani vimeshiriki kuibua mijadala ya kitaifa kupitia vikao vya rasmi vya bunge kukosoa serikali na chama tawala,sera, sheria, siasa, jamii, michezo, burudani,utamaduni na mingine inayogusa maeneo ya uchumi kuanzia sekta za madini.
Mathalani, hoja za mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mkoani Shinyanga, kwamba mkataba wake ulisainiwa nje ya nchi, iliyowasilishwa Bungeni na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe mwaka 2007, ambapo mwaka 2008 serikali ilitunga sheria ya fedha, ambayo ilirekebishwa kutokana na maoni ya Tume ya Jaji Mark Bomani na kwa madhumuni ya kuimarisha sekta ya madini mwaka 2010. Awali hoja ya Zitto ilipingwa vikali akiitwa mzushi kiasi cha kuadhibiwa kwa kusimamishwa kuhudhuria vikao kadhaa vya Bunge.
Hali kadhalika, aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia alisimama kidete kuhoji sera na ubora wa elimu kwa kuangazia namna mitaala inavyodidimiza sekta hiyo. Wakati Mbatia akifanya hayo alikuwa Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha NCCR Mageuzi aliyeteuliwa na rais awamu ya nne, Jakaya Kikwete wa chama tawala CCM kuwa mbunge katika kipindi chake cha pili na cha mwisho (2010-2015).
Mifano kama hiyo ya mbunge moja mmoja kuibua hoja na kushikilia msimmo wake ili mamlaka zitekleze jamabo fulani ipo mingi na imesaidia sana kurekebisha masuala ya msingi katika kuzingatia sharia na uwajibikaji.
Itakumbukwa kuwa Mwaka 1995 baada ya uchaguzi wa vyama vingi, wabunge wawili wa upinzani kupitia chama cha NCCR- Mageuzi, Mabele Marando na Masumbuko Lamwai, wote wanasheria kitaaluma waliibua hoja kupinga sehemu ya kiapo cha wabunge kilichokuwa na maneno ya wabunge kuapa kwa rais wa Tanzania badala ya kuapa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwishowe Spika wa Bunge wa wakati huo, Pius Msekwa alikubaliana na hoja ya wabunge hao hivyo kiapo hicho kikabadilishwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wakfu wa Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa rais wa Zanzibar, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipongeza mchango wa mwanasiasa huyo katika haki, amani, siasa na demokrasia kupitia vyama vya upinzani vya CUF na ACT Wazalendo. Mchango wa Maalim Seif ndiyo uliowakutanisha viongozi wa kitaifa kutoka vyama vya upinzani na chama tawala bila kujali tofauti za itikadi.
"Mara nyingi kwenye nchi zetu zinazoendelea wanasiasa wakitofautiana kinachofuata ni vurugu, lakini akiwepo mtu kama Maalim Seif vurugu hukatika na maridhiano yakaendelea, hii ni kwa sababu ama hakuna uthabiti katika misimamo ya hao Wanasiasa wanaoendeleza vurugu au hawako tayari kutafuta maridhiano na wanaotofautiana nao," alisema Rais Samia mnamo Novemba 5, 2021 wakati wa uzinduzi wa Wakfu huo.
Je vyama hivi vimedumu kwa muda gani hadi sasa?
Ni miaka 29 sasa tangu utawala wa Tanzania uliporuhusu tena siasa za vyama vya vingi nchini humo. Lakini ni miaka 26 tangu wananchi walipopiga kura kuwachagua viongozi wa nchi hiyo kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu uliovishirikisha vyama vya upinzani.
Julai mwaka 1992 serikali ya Tanzania iliutangazia ulimwengu kuwa imerejesha mfumo wa siasa za vyama vingi, kisha mwaka 1995 uchaguzi mkuu wa kwanza uliovishirikisha vyama vya upinzani ulifanyika. Matukio hayo muhimu katika maisha ya wananchi wa Tanzania yamefanyika ndani ya miaka 60 tangu ilipopata uhuru. Kwamba katika kipindi cha miaka 60 wananchi walishuhudia kufutwa siasa za vyama vingi wakati wa utawala wa rais wa kwanza wa nchi hiyo Julius Kambarage Nyerere aliyedumu madarakani miaka 24, kisha siasa hizo zikarejeshwa katika kipindi cha utawala wa rais wa pili, Ali Hassan Mwinyi chini ya Tume ya Jaji Francics Nyalali, huku Mwalimu Nyerere akiwa kinara wa kuunga mkono siasa hizo.
Manufaa ya vyama vya upinzani ni yaoi?
• Kukosa na kusaidia serikali kutolala usingizi wa pono katika uendeshaji wa nchi.
• Kupanua wigo wa majukwaa ya kidemokrasia na uhuru wa kuchagua kushiriki masuala ya siasa za nchi.
• Kuwa taasisi za kutengeneza wanasiasa na viongozi mahiri ambao baadhi wamehamia chama tawala na sasa wapo madarakani; David Silinde, Dk. Godwin Mollel,Mwita Waitara na Profesa Kitila Mkumbo kwa kuwataja wachache.
• Kushiriki harakati za maendeleo katika kila ngazi kuanzia kitongoji, kijiji, kata, tarafa, wilaya, kanda, hadi Taifa.
• Kushauri wananchi na watawala namna ya kujipatia fursa za maendeleo na ajira kwa kutumia elimu walizonazo, pamoja na kutoa elimu ya uraia kwa wanachama,wafuasi na wananchi wengine kupitia mikutano ya hadhara na ndani.
• Ni njia mbadala ya kutoa elimu ya uraia kwa wananchi.
• Huchochea serikali kusukuma maendeleo kwenye majimbo au Halmashauri zinazoongozwa na upinzani ili kupata ushawishi zaidi katika chaguzi zinazofuata.
• Kuimarisha siasa za ushindani miongoni mwa wananchi,wanasiasa na viongozi.
Gerard Nyerere, mtaalamu wa Teknolojia,uchumi na mchambuzi wa siasa na utawala bora nchini Tanzania, amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa vyama ya upinzani vimesaidia kuimarisha Taasisi za utendaji na weledi wa kiuongozi wa umma, na kwamba ni ni Taasisi muhimu katika jamii ya kidemokrasia na uhuru zaidi kwa wananchi nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment